RAMADHANI BROTHERS WALITEMBELEA HIFADHI YA TAIFA - SERENGETI
Washindi wa tuzo za American Got Talent, ambao ni wasanii katika mchezo wa sarakasi, Ramadhani Brothers walifikisha tuzo hiyo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti tarehe 07.04.2024 baada ya kuifikisha katika kilele cha Mlima Kilimanjaro tarehe 03.04.2024.
Hifadhi ya Taifa Serengeti ni hifadhi bora barani Afrika, ambayo imeshinda tuzo ya kuwa hifadhi bora Afrika mara tano (5) mfululizo.
Washindi wa tuzo za American Got Talent, ambao ni wasanii katika mchezo wa sarakasi, Ramadhani Brothers wakiwa wameshikilia tuzo zao juu mara baada ya kuzifikisha katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa lengo la kutangaza Utalii wetu ndani na nje ya nchi.
Wasanii hao walitembelea hifadhi hiyo kwa lengo la kutangaza utalii wa Tanzania ikiwa ni juhudi moja wapo za kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuutangaza Utalii duniani.
Mara baada ya kufika Mbugani Ramadhani Brothers walifanikiwa kufika eneo maarufu kama Makoma Hill, sehemu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alisimama na kuvua kofia wakati wa maandalizi ya filamu ya Tanzania The Royal Tour.
Mbali na hivyo pia, walitumia fursa hiyo kuonesha ufundi wao katika mchezo wa sarakasi ndani ya hifadhi ya Taifa serengeti kwa kupiga sarakasi eneo la Makoma Hill.
Wakizungumza mara baada ya kufika Serengeti, walifurahi sana na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya Tanzania pindi watakapokuwepo nje ya nchi.
“Kwanza kabisha tunamshukuru mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa, pili ni juhudi za kumuunga mkono Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya.
“Sisi Ramadhani Brothers tupo nyuma yake kwa kumuunga mkono kwa kulitangaza Taifa letu Kimataifa zaidi.
“ Usema ukweli tumefurahia sana kutembelea Hifadhi za Taifa, hususani hii ya Serengeti, tunawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya TANAPA, kulinda maliasili za Taifa letu nasi tutakuwa Mabalozi kutangaza vivutio vyetu tuwapo nje ya mipaka ya Tanzania,” walisema Ramadhan Brothers.
Vijana hao wazalendo wanaendelea kuhamasisha kampeni ya ‘votenow’ kwa ajili ya kupigia kura Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro zinazowania tuzo za World Travel Awards.